Saturday, March 9, 2019

WANAWAKE MSINYAMAZIE RUSHWA YA NGONO

Wanawake Mkoani Songwe wameaswa kutonyamazia vitendo vya rushwa ya ngono ili waweze kujikomboa kifikra, kiuchumi na kisiasa katika harakati za kufikia usawa wa kijinsia kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Akisoma hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela katika maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika Kimkoa Wilayani Ileje, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Palingo amesema rushwa ya ngono inapaswa ithibitiwe kwa nguvu zote
“Nawasihi sana wanawake wanaokumbana na udhalilishaji huu wa kuombwa rushwa ya ngono watoe taarifa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) pia wananchi wengine watoe taarifa mara tu wanapokutana na matatizo ya rushwa ili taasisi husika ziweze kushughulikia”, amesema Palingo
Ameongeza kwa kuziagiza halmashauri za Mkoa wa Songwe kuhakikisha zinaendelea kupiga vita unyanyasaji na ukatili wa kijinsia, taasisi zote zinazohusika na mapambano hayo ikiwa ni pamoja na dawati la jinsia kuwachukulia hatua wote wanaofanya vitendo hivyo.
Palingo ameelekeza kuwa halmashauri ziweke mazingira mazuri ya masoko ya bidhaa na mazao yanayozalishwa na wanawake, kutenga fedha kwaajili ya kuwawezesha wanawake kuwa na uwezo wa kumiliki viwanda na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake.
Akisoma risala kwa niaba ya wanawake Afisa Maendeleo ya Jamii Roida Kyomo amesema wanawake wamekuwa wakizalisha kidogo kutokana na ukosefu wa masoko, elimu na mitaji wakti uwezo wa kuzalisha bidhaa na mazao mengi wanayo.

Kyomo ameongeza kuwa uwepo wa mashauri 442 ya unyanyasaji wa kijinsia unaonyesha kuwa tatizo hilo bado lipo hivyo ameiomba serikali kuendelea kuhamasisha jamii kuachana na mila kandamizi kwa wanawake ili muda unaotumika katika kusuluhisha matatizo hayo utumike katika kuzalisha mali ili kukuza uchumi.


Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Palingo akionyesha Bidhaa zinazozalishwa na Kikundi cha wanawake wilayani Ileje.

HAONGA:SINUNULIKI KWA GHARAMA YEYOTE ILE


Mbunge wa Jimbo la Mbozi kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mh. Pascal Y Haonga. Amesema hanunuliki na yuko imara katika Jimbo lake na amejipanga vyema na uchguzi mkuu mwakani , Mh Haonga ametoa kauli hiyo jana alipokua akihutubia Wananchi wa Mji mdogo wa Mlowo.
Lakini pia, alitumia nafasi hiyo kumpongeza mkuu wa mkoa mpya wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus E. Mwangela kwa kumpa Ushirikiano katika kutumikia Wananchi.


Mbunge wa jimbo la Mbozi kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mh. Pascal Y Haonga akihutubia Wakazi wa Mji Mdogo wa Mlowo.
(picha na Amidu Mtalii)

Saturday, February 23, 2019

SALAMU ZA POLE


Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus E. Mwangela anatoa salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa ndugu, jamaa na marafiki wa wafiwa, kufuatia ajali ya gari iliyosababisha vifo 19 ikiwa wanaume ni 15 na wanawake wanne.
Brig. Jen. (Mst) Mwangela amesema kutokana na ajali hiyo iliyotokea usiku eneo la Senjele Wilayani Mbozi ikihusisha magari matatu yaliyokuwa yakielekea Mbeya kugongana, serikali Mkoani Songwe imetoa majeneza 19 pamoja na usafiri kwa ajili ya kuhifadhi miili ya marehemu.
“Rais Magufuli amenituma niwape pole na ametuelekeza kama Mkoa kusimamia Mamlaka za Usalama barabarani kufanya uchunguzi na hatua zinazo stahili kuchukuliwa, pia ameelekeza tujipange vizuri kukabiliana na matukio ya ajali za barabarani”, amesema Brig. Jen. (Mst) Mwangela.
Brig. Jen. (Mst) Mwangela amesema chanzo cha ajali hiyo kimetokana na gari la abiria aina ya coaster kugongwa na gari la mizigo lililokuwa nyuma yake kisha coaster kugonga gari la mizigo lililo kuwa mbele yake na kupelekea gari la abiria kubanwa katikati ya magari mawili ya mizigo.
Aidha ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, kuweka utaratibu maalumu wa magari kupita kwa kupokezana katika maeneo yote yenye miteremko mikali, kuwepo ukaguzi wa magari kabla hayajaanza kushuka au kupanda mlima pamoja na kuweka ulinzi wa maeneo hayo.


Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus E. Mwangela